Sunday, February 3, 2013




Mwanamke: Dalili zitakazomfanya mpenzi mpya akuone wewe ni king’ang’anizi…!

Hizi ni miongoni mwa sababu ambazo wanaume wengi huchomoa mapema kwa wapenzi wao wapya kabla uhusiano haujashika kasi. Kuna wakati wanawake hukosea na kuvuka mipaka mwanzoni tu mwa uhusiano. Anamganda mwanaume haraka sana au anaonesha dalili zote za kujipendekeza kupita kiasi. Lakini jambo ambalo wanawake wengi hawalijui ni kwamba, wanaume wako makini sana kuwakwepa wanawake ving’ang’anizi……..


Nitadadavua baadhi ya vijitabia vya wanawake vinavyowafanya wanaume wawaone kama ni ving’ang’anizi…..
1. Unataka kuwa naye muda mwingi kuliko kawaida… Ni vizuri kwa wapenzi wapya kupata fursa ya kuwa pamoja peke yao, lakini kama unakataa kuwa na mtoko, kuhudhuria sherehe au kukutana na marafiki na kulazimisha kuwa pamoja peke yenu mahali fulani pa faragha, basi hapo ni lazima mwanaume atadhani kwamba unataka akupe umuhimu wa pekee muda wote. Unaweza kukuta mwanamke anakuwa king’ang’anizi kiasi kwamba hana muda na marafiki zake au watu wengine isipokuwa mpenzi wake. Anakuwa kama mzigo, muda wote yuko nyuma ya mwanaume kila anapokwenda…. Hapa ni lazima mwanaume atatemana na wewe kungali mapema. Hakuna mwanaume anayeweza kujenga mahusiano na mwanamke wa aina hii, watakukimbia kila siku.

2. Unampangia mwanaume kila kitu… Unampangia aina ya mavazi ya kuvaa, unaanza kuboresha mazingira ya nyumbani kwake haraka sana kwa kununua vitu mbalimbali vya nyumbani kwake bila kushauriana naye. Hiyo ni dalili kwamba una matarajio makubwa kwake, jambo ambalo kwake yeye bado halijamuingia akilini. Hapa mwanaume ambaye huyachukulia mambo kwa tahadhari, hukuona kuwa wewe ni king’ang’anizi na unataka kukita mizizi kwake wakati bado anachunguza uhusiano wenu ili kujua iwapo utakuwa kama vile anavyotarajia yeye… Kumbuka kwamba kila mtu ana sifa azitakazo pale anapochagua mwenza, na ni vigumu kumjua mtu kwa muda mfupi. Kunahitajika muda wa kutosha mtu kumjua mwenzake vizuri linapokuja swala la mahusianao. 


3. Unatumia muda mwingi zaidi kukaa kwake…. Unalala kwa mpenzi wako, na asubuhi mwanaume huyo anaondoka kwenda kwenye shughuli zake, na wewe unabaki labda ukidai unamsaidia usafi kidogo. Lakini anaporudi jioni anakukuta bado uko hapo nyumbani kwake ukiwa umejipumzisha. Inawezekana ukawa umeandaa chakula cha usiku tayari na pia huenda ukawa umebeba nguo za kubadilisha kwenye mkoba wako pamoja na vipodozi ukiwa umejiandaa kulala tena hapo kwake. Huonyeshi dalili za kuondoka hapo kwake zaidi ya kwenda kwako au kwenu na kubadilisha nguo na kuchukua viti vichache utakavyovihitaji utakapokuwa hapo kwake, lakini unapanga hayo yote bila kumshirikisha zaidi ya kukuona tu ukimganda kama luba. Huonyeshi kuwa na maisha yako kama wewe, zaidi ya kujipachika kwake……


4. Unajenga urafiki na mama yake haraka sana…… Baada ya kukutambulisha kwa mama yake na kubadilishana namba za simu au labda na email, unaanza kujenga ukaribu na mama yake kupita kiasi. Wanawake wengi hudhani kwamba, iwapo watajenga urafiki na mama wakwe watarajiwa, basi itakuwa rahisi kwao kumnasa mwanaume huyo, maana huamini kwamba watoto wa kiume hawawezi kwenda kinyume na mama zao linapokuja swala la kuchagua mwenza. Kwa kawaida wanaume humuona mwanamke anayejipendekeza kwa mama yake kama vile anataka kulazimisha uhusiano au ndoa, hivyo humchukulia kama ni king’ang’anizi.




5. Unampigia simu na kumuuliza kama yuko wapi….. Unapompigia simu badala ya kumjulia hali unakuwa na maswali ya kipolisi.. ‘Uko wapi?’ ‘Unafanya nini? Maswali ya aina hiyo mwanaume huyachukulia kama ya kimtego na hawafurahishwi nayo. Wanawake wengi huamini kwamba wanaume huwa hawasemi ukweli kuhusu mahali walipo pale wanapoulizwa na wenzi wao. Jambo hilo linaweza kuwa kweli au lisiwe kweli. Inawezekana kuwa kweli kwa sababu labda ya wanaume kukwepa maswali mengi. Mara nyingi wanawake hawaridhiki na jibu moja. Mfano ni jioni ndio ametoka kazini, lakini nakapitia mahali fulani kukutana na rafiki yake, inawezekana ikawa ni kwenye mghahawa au kwenye baa. Kama mwanamke akipiga simu na mwanaume akamwambai yuko kwenye baa na rafiki yake, yatafuata maswali lukuki. Hakuna mwanaume anayependa kuulizwa maswali mengi kama vile anatuhumiwa. Na ndio sababu wanaume wengi wanakwepe kusema mahali walipo. Kwa hiyo ili kuepuka maswali anaweza kujibu kwa kifupi tu kwamba yuko kwenye kikao kazini na hatakuwa hewani, ili apate nafasi ya kuzima simu japo kwa muda. Mwanaume humuona mwanamke mwenye udadisi wa aina hiyo kama king’ang’anizi. 


6. Unakuwa na chuki na wanawake wenzako… Pale ambapo mwenzi wako anapomtaja mwanamke fulani, inaweza kuwa ni mfanyakazi mwenzake, mke wa kaka yake au mtu wanayeshirikiana kibiashara, unaonyesha kisirani cha waziwazi kwamba unakerwa na ukaribu wake na wanawake wengine. Tabia hii inaashiria kwamba wewe unapenda kumiliki na wanaume wengi huwa hawapendi wanawake wenye vijitabia vya kupenda kumiliki. Hapo ni lazima utaonekana kuwa wewe ni king’ang’anizi na uhusiano wenu utavunjika mapema…..

7. Unakubali kila analosema au kila anachokifanya….Kuna kitu kinaitwa ‘uhusiano wa kinyonga.’ Hapa mwanamke anajibadili kupita kiasi ili afanane na mwenzi wake. Unakuta mwanamke anakubali kila kitu anachokiamini mwenzi wake bila kuhoji. Anapoteza utambulisho wake na kujipachika utambulisho wa mwenzi wake. Mwanaume akikuona uko hivyo, atakukimbia, atajua wewe ni king’ang’anizi
8. Unawazungumzia mabwana ulioachana nao kila wakati…Kama una kawaida ya kumzungumzia mwanaume uliyeachana naye mara kwa mara uwapo na mpenzi wako mpya, ina maana kwamba bado hujaachana na jakamoyo la kuachwa. Hakuna mwanaume anayependa kusikia kuhusu mahusiano yako ya nyuma, kwa sababu hayamuhusu. Kama ukiwa unapenda kumzungumzia mpenzi wako wa zamani kila uwapo na mpenzi wako mpya, jua kwamba na yeye pia utampoteza kwa sababu atakuona kuwa wewe ni dhaifu na king’ang’anizi na ndio maana umeshindwa kusimama kama wewe, na badala yake unawaza kuhusu mtu uliyeachana naye pamoja na kwamba uko naye. Sio kwamba ni vibaya kumzungumzia mpenzi mliyeachana, lakini ni vyema kama utamzungumzia pale ambapo kuna ulazima sana wa kufanya hivyo, labda kuna jambo ambalo limamhusu ambalo mnajadili, na ikakulazimu kumtaja…..

SIYO KILA DALILI YA MWANAUME KUPENDA NI YA KWELI....!


Siyo kila dalili ya mwanaume kupenda ni ya kweli…!


Kuna wakati ambapo, wanawake wanajikuta wakikabiliwa na swali la, je, mwanaume huyu ananipenda kweli? Hii hutokea pale anapokutana na mwanaume ambaye, huenda amevutiwa naye. Pengine mwanaume naye anaweza kuonesha kuvutiwa na mwanamke huyo.

Kwa hiyo, mwanamke hujiuliza kama akubali ombi la mwanaume huyo na kukubali kuzungumza naye au kuanzisha naye uhusiano, kama mwanaume atakuwa amezungumza naye kuhusu jambo hilo. ni kweli kwamba, kuna ugumu kwa mwanamke kujua hasa ni kwa namna gani anaweza kujua kwamba, huyo mwanaume amempenda kweli au hapana.

Kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa ni dalili ya kumpenda mwanamke, lakini wakati huo huo vinaweza visiwe.

1. Hebu tuchukulie kwamba, mwanaume ameonesha kuwa na tabia tunazoziita nzuri. Labda amekumbuka kirahisi jina la mwanamke, ameonesha kuwa msikilizaji mzuri, ameonesha kuwa anajali kuhusu kinachosemwa na mwanamke, na amekuwa anamuuliza maswali kwa dhati na utulivu. Hapa mwanamke anaweza kuamini kwamba, huyu mwanaume anampenda. Lakini ukweli huenda ukawa ni kinyume chake. Inawezekana huyo mwanaume ni muungwana tu, na anaonesha tabia hizo kutokana na uungwana wake na siyo kutokana na kumpenda kimapenzi mwanamke.

2. Kuna watu ambao wana upendo, wamekomaa kihisia na wanajua kuhusiana vizuri na watu. Hii haina maana kwamba, kumwonesha mtu tabia hizo, kuna maana ya kumpenda au kumpenda sana mwanamke. Dalili hizi ni nzuri na inawezekana zikawa zinaonesha mwanaume kumpenda mwanamke, lakini mwanamke asilichukulie jambo hilo kwa namna hiyo.

3. Mwanaume anaweza kuonesha kuwa na udadisi kuhusu mwanamke kwa maana kwamba, kutaka kujua mambo yake, kumfuatilia au kuulizauliza kuhusu habari za mwanamke. Hii haina maana kwamba mwanaume amempenda kimapenzi. Inawezekana mwanaume akawa amevutiwa kimapenzi na mwanamke ndiyo maana akaonesha tabia hizo, lakini siyo lazima iwe hivyo. Kumbuka kwamba, mwanaume anaweza kuvutiwa na mazungumzo ya mwanamke, akavutiwa hata na namna alivyo usoni, hivyo akapenda kuzungumza naye lakini siyo kwa sababu anampenda.

4. Kuna wanaume ambao wana wake au wapenzi, lakini wanajisikia vizuri kusikiliza wanawake wengine au kujua tu habari za wanawake wengine, bila kuwa na haja ya kuanzisha uhusiano nao. Mwanaume anapompa mwanamke ‘ofa’ hasa ya chakula cha mchana au usiku, ni dalili ya wazi ya kuvutiwa naye. Hapa kuna uhakika mkubwa zaidi, labda tu kama mazungumzo yanayotajwa kufanywa wakati huo wa chakula yanafahamika, na ni ya shughuli maalum. Kwa hiyo ‘ofa’ ya chakula ni dalili nzuri na yenye uhakika. Lakini kuna jambo ambalo ni muhimu kwa mwanamke kulifahamu katika hali kama hii. Kuna wakati mwanaume kumpa ‘ofa’ mwanamke kwa chakula cha mchana au jioni, kunaweza kusiwe na maana ya moja kwa moja kwamba, uhusiano utaundwa. Inawezekana katika kutoka outing huko, mwanaume akaghairi. Kwa wengine huchukua muda hadi kuamua kuhusu kuunda uhusiano au hapana.

5. Hata mwanaume kuamua kumpeleka mwanamke kwa familia yao na kumtambulisha kama rafiki yake, ni hatua yenye kuonesha kwamba, mwanaume ameamua kumpenda mwanamke huyo. Lakini wakati mwingine hii inaweza ikawa ni janja yake kutaka tu kumthibitishia mwanamke ili amhadae vizuri, na wala hakuna maana ya uhusiano wa kudumu.

6. Kuzungumza kwa pamoja kuhusu masuala ya baadaye ya kiuhusiano, kama vile, idadi ya watoto na mambo mengine ambayo mara nyingi huzungumzwa na watu ambao tayari wako kwenye uhusiano ni dalili ya mwanaume kuvutiwa mwanamke. Lakini tatizo la jambo hili ni kwamba, kuzungumza masuala ya baadaye inaweza kuwa ni njia ya mwanaume kutaka kujisikia au kujua jinsi inavyokuwa katika mambo hayo. Inaweza kuwa pia ni njia yake ya kutaka kupima wanawake wanavyosema kuhusu masuala hayo. Lakini inaweza ikawa mwanaume huyo anatafuta kujua misimamo ya mwanamke huyo ili hatimaye afanye uamuzi. Kwa hiyo, bado haioneshi kuwa amevutiwa na kuamua tayari.

Mara nyingi wanawake hudanganywa na dalili fulani zinazooneshwa na wanaume wakati wanapoanza kuzoeana nao. Dalili hizi huwafanya kuamini kwamba, wanaume hao wamewapenda tayari, wakati siyo kweli. Kwa kuangalia baadhi ya dalili hizo kama nilivyozitaja, mwanamke anaweza kuwa makini wakati anapoanzisha uhusiano, ili asikurupuke na kujikuta amedanganyika. Ni kweli, kuna wakati ni dalili zinasema kweli, lakini kuna wakai zinadanganya kuhusu kupenda au kupendwa.

JUL 26, 2013

WANAUME HAWAOI SURA TENA BALI UELEWA....!

Wanaume hawaoi sura tena bali uelewa…!

Siku za nyuma, wanaume walijali zaidi uzuri wa sura na mwili wakati walipokuwa wanatafuta mke. Lakini utafiti uliofanywa duniani kote unaonesha kwamba, wanaume hivi sasa wamebadili mitazamo na kuanza kuangalia vitu vilivyo zaidi ya uzuri wa sura na mwili.


Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Grand Valley kilichopo jimboni Michigan nchini Marekani walioendesha sehemu kubwa ya utafiti huo wamesema, wanaume hivi sasa wameanza kujali uwezo wa wanawake katika kufikiri na kujua namna ya kujenga maisha kuliko kujali sura zao na maumbile.



Tafiti nyingi, ukiwemo huo wa karibuni wa Chuo cha Grand Valley, zinaonesha kwamba, kwenye miaka hadi 1980, wanaume walikuwa wakioa wake ambao wanaume hao wanawazidi kielimu na hata kimapato. Lakini kufikia mwaka 2002, wanaume wengi walikuwa wameoa wanawake ambao wanawazidi kielimu, kimapato au kukaribiana.



Lakini pia imebainika kwamba, hadi kufikia miaka hiyo, wanaume na jamii nyingi zilikuwa zikimtazama mwanamke anayefaa kuolewa kuwa ni yule mzuri sana kwa sura na umbo. Lakini kufikia mwaka 2002, wanaume wengi na jamii walikuwa wanaamini kwamba, mwanamke mwenye uwezo mkubwa wa kuelewa maisha ndiye anayefaa kuwa mke.
Kwa miaka ishirini hali imebadilika sana. Maisha yamezidi kuwa magumu na uhitaji wa watu kusaidiana katika kuyakabili umeongezeka. Kwa hiyo mtu anapofikiria kuoa huanza kujiuliza atakavyomudu maisha na mke. Kwa hofu za kushindwa, hujikuta akijiuliza namna atakavyoweza kusaidiana na huyo anayetaka kumwoa katika kufanya mambo yaende.


Siku za nyuma, mwanamke mwenye kipato kizuri alikuwa katika ugumu wa kupata mume, lakini siku hizi, bila kujali sura au sifa nyingine, uhakika wa mwanamke kuwa na njia za kipato unampa, nafasi kubwa zaidi ya kuolewa. Kilichokuwa kinaogopwa huko nyuma na wanaume kwa sasa ndicho kinachokimbiliwa.



Tafiti hizo zinasisitiza kwamba, thamani ya mwanamke kwenye jicho la mwanaume inaanza kuondoka kwenye uzuri wake wa sura na mwili na kuingia kwenye uwezo wake katika kuyakabili maisha. Hii ikiwa na maana kwamba, kwa kadiri siku zinavyoenda, wanawake ambao watakuwa na nafasi kubwa ya kuolewa watakuwa ni wale waliosoma au wale wenye shughuli za kuzalisha.

Wataalamu wengi wanasema, hivi sasa uzuri unaonekana kabisa kubadilishana nafasi na elimu na uwezo wa ‘kutafuta maisha’ wa mwanamke. Kwa hiyo, sasa siyo suala la uzuri tena, bali mwanamke anajua kitu gani na ana uwezo kiasi gani wa kufanya maisha yawe bora sana.


Hii pia ina maana kwamba, dhana ya zamani ya mwanamke mzuri kuolewa na mwanaume msomi au mwenye fedha imeanza kukosa mashiko. Siku za nyuma mwanamke mzuri sana, angeolewa na mwanaume mwenye fedha, kama zilivyo bidhaa nzuri kuangukia mikononi mwa wenye uwezo kifedha.



Lakini leo hii, wanaume wanachoweza kufanya ni kuwachezea kimapenzi wanawake wazuri na siyo kuwaoa. Linapokuja suala la kuoa, kisomo na uwezo wa kuyajua maisha huchukua nafasi. Uzuri wa sura hubaki nyuma kwanza.

WANAUME WENYE WAKE WAZURI, HUWA NA 'NYUMBA NDOGO' ZISIZOTAZAMIKA KWA SURA AU UMBO.....!

Wanaume wenye wake wazuri, huwa na ‘nyumba ndogo’ zisizotazamika kwa sura au umbo…..!

Kwa mujibu wa utafiti wangu nilioufanyia kwenye eneo langu la kazi na kwa majirani zangu nimebaini kwamba, kati ya wafanyakazi watano niliofuatilia nyendo zao, ni wawili ambao walikuwa na ‘nyumba ndogo’ nzuri na zenye mvuto kuliko wake zao. Watatu walikuwa na ‘nyumba ndogo’ ambazo zinaweza kumpelekea mtu kujiuliza inakuwaje mwanaume huyo kuwa na ‘nyumba ndogo’ hiyo ambayo hata kwa mbali sana haiwezi kulingana na mkewe. Kwa jirani zangu wanne hali haikuwa nzuri, kwani hapa watatu walikuwa na ‘nyumba ndogo’ zilizo kinyume na wake zao kwa sura na umbo.

Watu saba niliowahoji kuhusu jambo hili, watatu walisema kwamba, wana ushahidi kuhusu wanaume wanaowafahamu wenye ‘nyumba ndogo’ zisizotazamika ukilinganisha na wake zao. Wengine wanne walitoa ushahidi wa wanaume wanaowafahamu ambao wana ‘nyumba ndogo’ nzuri sana ukilinganisha na wake zao.


Ni kitu gani kinatokea?


Ni kwamba, kuna ukweli kuwa wanaume wanaweza kuacha wake zao wazuri sana nyumbani na kufuata wanawake wabaya wasiotazamika kwa sura na umbo huko nje. Lakini pia wanaweza kuacha wake zao wabaya kwa sura ndani na kwenda kufuata wanawake wazuri kwa sura na umbo huko nje.

Hii ina maana gani?

Hii ina maana kwamba kuna mkanganyiko kwenye jambo hili. Lakini kwa bahati nzuri mkanganyiko huu kamwe siyo mkubwa na unaoweza kuumiza kichwa cha mtu. 


Binadamu ana kitu kiinachoitwa ukinaifu. Ukinaifu ni hali ya mtu kuchoka kukiona kitu kilekile mara zote. Kwa mfano, mtu anaponunua nguo mpya leo huipenda sana. Lakini baada ya muda fulani, ikiwa bado haijachakaa hujikuta kiwango cha kuipenda kikishuka.

Lakini ni vizuri nikarudi nyuma na kusema kwamba, kwenye suala la mapenzi. Ukinaifu huwapata wanaume kuliko wanawake. Inawezekana sababu ni za kimaumbile na hivyo ni vigumu kusema ni kwa nini inakuwa hivyo.


Kwa sababu ni suala la kimaumbile inakuwa kama lazima kwa mwanaume kupata ukinaifu. Anapopata ukinaifu siyo lazima atoke nje, yaani dawa yake au ufumbuzi siyo kutoka nje ya ndoa, ingawa wanaume wengi hufanya hivyo. Wanapofanya hivyo siyo kwamba, wanajua kwamba, wamepata ukinaifu, hapana. Wao hudhani tu kwamba, wamempenda mwanamke fulani kwa sababu hizi au zile.
Nadharia moja kuhusu ukinaifu ni kwamba, ili ukinaifu ushibishwe ni lazima mtu apate kitu kilicho kinyume na kile ambacho kimempa ukinaifu huo, au kuwa nacho mbali kwa muda fulani. Kwa mfano, kama mwanaume amepata ukinaifu wa umbile la mkewe ambaye ni kimbaumbau, ni lazima kama ataamua kwenda kutafuta mwanamke wa nje, atatafuta mwanamke tipwatipwa.

Kwa mkabala huo, ndiyo pale tunapokuta mwanaume akimfuata mwanamke wa nje mbaya ukilinganisha na mkewe. Labda anaamua kumfuata mwanamke huyo kwa msukumo wa ukinaifu – amekinaishwa na umbo au sura ya mkewe na hivyo angetaka kuona sura ya aina nyingine, ili afute ukinaifu wake. Kinyume cha sura nzuri ni sura mbaya, kwa hiyo atatafuta mwanamke mwenye sura kinyume na ile ya mkewe.
Kuna ukinaifu wa aina nyingi kwenye maisha ya ndoa. Mwanaume anaweza akakinaishwa na mtindo wa nywele wa aina moja wa mkewe. Kama mwanaume huyu hatakuwa mwangalifu, atajikuta akitafuta ‘nyumba ndogo’ yenye mtindo tofauti na mkewe. Inawezekana mkewe anatumia mtindo wa ‘twende kilioni’ kila akisuka nywele zake. Mwanamume anapokwenda kutafuta kilicho kinyume huko nje, anaweza akajikuta amevutiwa na mwanamke mwenye kunyoa na kuchana nywele zake fupi.

Kwa hiyo, inawezekana kabisa mwanaume akatoka nje ya ndoa yake kutafuta kinyume ambacho siyo sura wala umbile. Inawezekana akatoka kwa sababu amekinaishwa na ukimya wa mkewe, hivyo anatafuta kelele. Huyu anaweza kujikuta akiwa na mwanamke wa nje muongeaji na chakaramu sana, ambaye kisura na kiumbile anaweza kuwa sawa na mkewe.

WANAWAKE: WANAUME WANAPOWABISHIENI MSIWASHANGAE...!

Kwa nini wanaume ni wagumu sana kufanya mambo ambayo wake zao wanawaomba au kuwataka kufanya? Jibu, ni kwa sababu ni wanaume na wameona baba zao wakifanya hivyo na wakaiga. Lakini jibu linaweza kuwa lingine, kutegemea na ufahamu wa mtu na hata mazingira. Lakini ukweli unabaki kwamba wanaume sio wepesi wa kutenda yale ambayo wanatakiwa na wake zao kutenda. 

Taarifa za kiutafiti zinaonesha kwamba, mwanaume ni mgumu kufanya anayotakiwa au kuombwa na mkewe kufanya kwa sababu nyuma ya ubongo wake, kuna kizuizi. Inadaiwa kwamba ubongo wa kina wa mwanaume kuna kitu kinachopingana na chochote ambacho mwanamke anamtaka kufanya.



Siyo suala la kurithi, hapana. Ukweli ni kwamba, kutokana na mwanaume kutokuwa tayari kuongozwa au kumsikiliza mwanamke na kumkubalia, hatimaye imejijenga akilini na kuwa kama vile ni suala la maumbile. Ukweli ni kwamba, miaka mingi ya kutoamini kwamba, mwanamke anaweza, imefanya kuwe na kizuizi hicho kwenye akili ya mwanaume.

Utafiti wa hivi karibuni kwa mfano, ambao uliongozwa na Gavan Fitzsimons profesa wa masoko na saikolojia, kwenye chuo kikuu cha Duke, anasema, kinachotokea ni juhudi za mwanaume kutotaka kuingiliwa kwenye mambo yake, bila mwenyewe kujua kwamba, anafanya juhudi hiyo. Jambo hili kisaikolojia linafahamika kama reactance, ambapo mtu hufanya kinyume kabisa na anavyotakiwa kufanya. Ni juhudi za mtu kupinga kupewa amri au kuingiliwa katika uhuru wake. 

Wataalamu wanasema kwamba, wanaume hujikuta tu wamepinga jambo la mke bila kujua hata sababu. Ndio maana wanaume wengi huharibikiwa kwa kukataa kufanya yaliyopendekezwa na wake zao na baadae hujiuliza ni kwa nini walikataa. Kwa hiyo wanaume wanapaswa sasa kujua kwamba, wanapombwa jambo na wake zao au kutakiwa kulifanya, wako kwenye hatari ya kulikataa. Kwa hali hiyo, wanapaswa kuwa waangalifu.

JUL 10, 2013

MWANAMKE: JE UNATAFUTA MCHUMBA? FUATA KANUNI HII, HAKIKA UTAMPATA MCHUMBA MWENYE TABIA UZITAKAZO


Mwanamke: Je, unatafuta mchumba? Fuata kanuni hii hakika utapata mchumba mwenye tabia uzitakazo...

Kuna kitu kinaitwa nguvu ya mvuto, lakini pia huenda mmeshawahi kusikia au kusoma kitabu kinachoitwa “The Secret.” Ni kitabu kizuri sana kinachoeleza kwa kirefu na kwa lugha nyepesi inayoeleweka jinsi nguvu hii ya mvuto inavyofanya kazi. Katika kitabu cha The Secret mwandishi Rhonda Byrne anasema kwamba mawazo yetu ni kama sumaku. Kwa kawaida sisi wanadamu tumezungukwa na nguvu ambazo hatuzioni lakini zipo kwa hiyo Kwa jinsi tunavyofikiri hayo mawazo yanakuwa na nguvu ambazo zinavuta kila kitu tunachowaza, kiwe kizuri au kibaya, ni lazima kitarudi kilipotoka, ambapo sipengine bali kwako wewe mwenyewe.

Rhonda anazidi kubainisha utendaji wa mawazo yetu kwa kutoa mfano wa ufanyaji kazi wa Luninga (TV). Kama wote tunavyofahamu kuwa ili kituo cha kurusha matangazo ya Luninga kifanye kazi kunakuwa na minara inayosafirisha mawimbi na kuyageuza katika mfumo wa picha na hivyo kutuwezesha kuona matangazo ya luninga tukiwa majumbani kwetu. Wengi wetu hatufahamu mitambo hiyo inafanya kazi namna gani, lakini tunafahamu kwamba kila chaneli ina mawimbi yake ambapo kila tukichagua chaneli fulani tunapata picha katika luninga zetu. Tunachagua mawimbi kwa kubadilisha chaneli na ndipo tunapopata picha za matangazo kutoka katika chaneli hiyo. Kama tunataka kuona picha na matangazo tofauti katika luninga zetu tunabadilisha chaneli kwa kutafuta mawimbi ya chaneli nyingine.

Sisi kama wanaadamu tuko sawa na mnara wa kurusha matangazo ya luninga na tuna nguvu kuliko minara ya kurusha matangazo iliyowahi kuwepo hapa duniani. Mawimbi yetu ndiyo yanayoratibu maisha yetu na ndiyo yanayoifanya dunia iwe kama livyo leo, kwani tunatengeneza mawimbi kutokana na namna tunavyowaza. Ile picha tunayopata au tunayoiona kupitia mawazo yetu, sio sawa na ile tunayoiona katika luninga zetu sebuleni kwetu, bali ni picha ya maisha yetu! Mawazo yetu yanatengeneza mawimbi na yanavuta kila tunachokiwaza na kuwa ndio maisha yetu halisi.

Iwapo tunataka kubadili chochote katika maisha yetu, basi inatulazimu tubadili chaneli na mawimbi kwa kubadili namna yetu ya kufikiri. Mwandishi huyo anaendelea kusema, kinachosabisha watu wengi wasipate kile wanachokitaka maishani ni kwa sababu wanafikiria zaidi kuhusu kile wasichokitaka badala ya kile wanachokitaka. Hebu tujaribu kuchunguza mawazo yetu na kauli zetu, tutagundua siri kubwa. Kwani nguvu ya mawazo ipo na inafanya kazi. Ugonjwa mkubwa sana unaowakabili wanadamu hapa duniani karne kwa karne ni ugonjwa wa “sitaki” au “sipendi,” anabainisha mama huyo. “Watu wameendelea kuacha ugonjwa huu uendelee kutawala katika mawazo yao, vitendo vyao na kauli zao, wakiendelea kuzingatia yale wasiyoyataka au wasiyoyapenda.” Anamalizia kusema mwandishi huyo.

Ugonjwa huo ndio unaowatesa baadhi ya wanawake wanaotafuta wapenzi. Mfano halisi ni kauli kama, “mimi sipendi wanaume wafupi,” au “mimi sipendi kuolewa na mwanaume mnyanyasaji….” na kauli nyingine zinazofanana na hizo. Ukweli ni kwamba kitakacho watokea wanawake wenye kutoa kauli kama hizo ni kuishia kuolewa na wanaume wa aina hiyo….. kinachofanyiwa kazi na mawazo yetu ya kina (Unconscious Mind) ni kile tunachokitamka, iwe ndicho tunachokitaka au tusichokitaka, mawazo yetu ya kina hayajui neno sipendi au sitaki, hukuletea kile ulichokitamka na kukijaza katika akili yako. 


Kuna wanawake wengi ambao wameolewa au wamewahi kujenga mahusiano na wanaume ambao waliwahi kutamka hadharani kwamba kamwe hawatoweza kujenga mahusiano nao au kuolewa nao. Hayo ni matokeo ya kauli zao ambazo walizitamka bila kujua madhara yake. Kwa hiyo basi kwa kutumia kanuni hiyo ya mvuto kama alivyosema mwandishi Rhonda Byrne mnatakiwa kuanza kuratibu mawazo yenu na kauli zenu kwa kutamka aina ya wanaume ambao mngependa kujenga mahusiano nao au kuolewa nao na haiishii hapo ni vyema mkajiweka katika mazingira ambayo yatawavuta kuelekea mahali ambapo mtakutana na aina ya wapenzi muwatakao. Huwezi tu kukaa nyumbani kwako au kutembelea eneo moja hilo hilo kila siku halafu utarajie kukutana na aina ya mpenzi umtakaye itakuwa ngumu, labda uwe na bahati sana.

MWANAMKE: KABLA HAJATOA TAMKO LA KUFUNGA NDOA USIMWAMBIE HAYA...


Mwanamke: Kabla hajatoa tamko la kufunga ndoa usimwambie haya…!


Katika maisha wote tuna siri zilizotuzunguka na mambo mbalimbali ya kifamilia pengine yanayotia kinyaa ambayo huwa tunatamani yasijulikane kwa wengine au labda yafutike kabisa. Lakini inategemea unayachukuliaje mambo hayo au yanaathiri vipi mitazamo yako kuhusu wewe. Ukweli ni kwamba hatuwezi kuyabadili labda tunachoweza kufanya ni kubadili mitazamo ya wengine kuhusu yale yaliyotuzunguka…………

Familia yenu ni ya vurugu tupu:
Baba yako ni mlevi kupindukia au baba yako na mama yako wote ni walevi kupindukia. Kaka zako ni mateja au dada zako wote wamezalia nyumbani au waliwahi kuolewa na kuachika, na sasa wako nyumbani tu wakichapa umalaya na pengine wanaendelea kuzalia nyumbani. Haya ni mambo ambayo hupaswi kuyazungumzia kwa mpenzi ambaye hajatoa tamko la kutaka mfunge ndoa. Kwani itamfanya mpenzi mpya atengeneze tafsiri tofauti kuhusu wewe. 

Uhusiano wako wa mwisho na mwenzi wako ulivunjika kwa vurugu:
Inawezekana mpenzi wako wa kwanza mliachana kwa vurugu kubwa, kwa mfano ulifikia hatua ya kufanya jaribio la kunywa sumu kutokana na kugombana kwenu kabla ya kuachana kwenu. Haya ni mambo ambayo hupaswi kuyasema kwa mpenzi wako mpya, kwani utampa maswali mengi sana ya kujiuliza juu yako.

Idadi ya wapenzi uliowahi kuwa nao:
Kuwa na idadi ndogo au kubwa ya wanaume uliowahi kuwa na uhusiano nao haimaanishi kwamba wewe ni mzuri katika mapenzi, sana sana unajidhalilisha tu. 


Maisha yako ya ujanani ya kujirusha:
Maisha yako ya ujanani au ulipokuwa shule ukijirusha kwenye kumbi za starehe ni ya kwako na si vyema uyapigie upatu kwa mpenzi mpya ili akujue kwamba na wewe hauko nyuma katika mambo ya starehe.


Ushawahi kuishi maisha ya kutangatanga:
Ni kumbukumbu yenye kuumiza hisia pale ukumbukapo maisha yako ya utotoni kama yalikuwa magumu na machungu. Kulelewa na wazazi wasiojali na watesaji, kuishi kwa kutangatanga kutoka nyumba moja hadi nyingine kutafuta hifadhi kutokana na kunyanyaswa. Kubakwa au kuishi maisha ya vurugu katika familia. Haya ni matukio ambayo yameshapita na hayatakiwi yatawale fikra zako tena. Umeshakua mtu mzima na maisha yanasonga mbele. Kuanza kumsimulia mpenzi mpya kuhusu aina ya maisha uliyokulia kama yalikuwa ni ya taabu kama nilivyoeleza hapo juu kutamfanya akuone kama wewe utakuwa unatonesheka kihisia haraka kutokana na kujeruhiwa kihisia utotoni. Mpenzi anaweza kukukwepa na hatimaye kukukimbia.

JUL 8, 2013

HII NDIYO SABABU YA WANAWAKE WENGI KUIBUA MABOMU...!

Hii ndiyo sababu ya wanawake wengi kuibua mabomu…!

Mnamo mwaka 1973 Dk. Paul MacLean, mtafiti toka taasisi ijulikanayo kama National Instute of Mental Health, alibaini kwamba, ubongo una sehemu tatu zinazoendana na nyakati tatu za mabadiliko ya kimaumbile.

Sehemu ya kwanza inaitwa reptilian. Hii inahusiana na kukutana kimwili kati mwanamke na mwanaume na tabia ya ukatili, hisia za hasira na hofu. Sehemu ya pili ni limbic brain. Hii inahusika na mapenzi, huzuni na wivu. 

Hata matumaini asili yake ni katika sehemu hii. Sehemu hii ndiyo inayodhibiti mapigo ya moyo na joto. Yote haya huathiriwa na kuwepo mahali hapo na mtu tunayempenda. Hamu ya mapenzi huenda moja kwa moja katika sehemu hii. Ni sehemu ambayo ina pupa na inaenda kasi kama umeme.

Ni enao ambalo halitaki kabisa kujishughulisha na mambo ya kutumia akili au tathmini. Sehemu ya tatu ya ubongo inaitwa neo-cortex, ambayo huruhusu matumizi ya mantiki, kutafakari kwa kina, lugha, kufanya mipango, kufikiri na maamuzi ya kina baada ya kufikiri kwa kina.

Katika kitabu chake cha The Emotional Brain, Joseph LeDoux anasema kwamba, sehemu zile mbili za kwanza za ubongo zinathibiti sana ile sehemu ya tatu. Na wala hii sehemu ya tatu haina udhibiti kwa zile sehemu mbili. Na ndiyo maana katika maisha ya kawaida, ‘hisia hudhibiti fikra.’ 

Ingawa fikra zinaweza kuamsha hisia kirahisi, lakini fikra zinapata tabu sana kuziondoa hisia zikishaingia. Hii ina maana sehemu ya pili ambayo ndiyo inayoziamrisha hisia, inaweza kuiburuza sehemu ya tatu kila inapotaka. Limbic ya mwanamke itamwambia, “umempata mwanaume barabara.” Sawa, lakini mwanaume mwenyewe ni mlevi..! 
Limbic itasema, “Nitaishi naye hivyohivyo. Ana sura nzuri mno, ninajisikia vizuri sana ninapokuwa naye….”


Sasa nafikiri unaweza kuona kwamba, hata kama mwanamke anaweza kusema kwamba anamtaka mwanaume mwenye haiba nzuri na mtu mwema si lazima kwamba, ndiye atakayevutiwa naye. Mfano mzuri wa jambo hili ni chakula.

Je huwa tunakula chakula kufuatana na ubora wake kiafya? Hapana…! Wengi wetu tunakula kutokana na utamu na ladha ya chakula! Dona ni bora kuliko ugali wa mahindi yaliyokobolewa kiafya. Lakini asilimia 90 ya Watanzania wanapenda ugali wa mahindi yaliyokobolewa maarufu kama Sembe. 

Hali hii ndiyo inayompata mwanamke anapofanya uchaguzi na kujikuta akimchagua mwanaume anayemfanya kujisikia raha, lakini ambaye si mtu mzuri kwake.

Suluhisho la jambo hili ni nini….?

Wanawake wanaweza kufanya urafiki na wanaume hao wazuri wa sura na wenye sifa ya uburuzaji na valuvalu kwa idadi wanayotaka kama kwa kufanya hivyo watajisikia raha maishani mwao; ili mradi tu urafiki huo usilete maumivu na huzuni ambayo yako juu kuliko furaha yenyewe. 

Kama huzuni ni kubwa kuliko furaha katika mapenzi na mwanaume aliye naye, basi mwanamke hana budi kuachana na limbic brain na kuchagua mwanaume anayemfaa kwa kutumia mantiki.

KWA NINI WANAUME WENGI SIKU HIZI HAWAPENDI KUOA...?

Kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuaje vijana wa kiume wamekuwa ni waongo sana hasa linapokuja swala la kuoa? Kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inazidi kuongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.

Kwa nini hali hiyo hutokea?

Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hilo, lakini yapo mambo ambayo yanaweza kutupa angalau tafakuri. Nitajaribu kudadavua baadhi ya sababu zinazowafanya wanaume siku hizi kukwepa kuingia katika taasisi ya ndoa:

Ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano: Hapa nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa malezi ya upande mmoja yaani walilelewa na mama peke yao. Sina maana ya kudharau au kutweza malezi ya mama, la hasha, lakini ni vyema mkafahamu kwamba kuwa na baba asiye na malezi mazuri si sawa na kutokuwa na baba. Na ndio maana nikasema ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano. Achilia mbali aina ya malezi atakayoyapata kwa familia yawe mazuri au mabaya lakini lazima kutakuwa na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto wa kiume katika familia husika. Watoto waliolelewa na mama peke yao kuna kitu huwa wanakosa, kwani wanakuwa hawana mtu wa kumchukulia kama mfano kwa upande wa jinsia ya kiume na hapo ndipo hujikuta wakijifunza wenyewe namna ya kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika makuzi yao hawakupata fursa ya kuwa karibu na baba zao. Kwa kuwa siku hizi kuna kundi kubwa la kina mama ambao wamejikuta wakiachiwa mzigo wa malezi ya watoto, baada ya aidha kuachwa na waume zao au kuzalishwa na kutelekezwa (Single mothers), na hapo ndipo tunaposhuhudia mtoto wa kiume anapokua kwa umri na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia kama mfano wa mume anavyotakiwa kuwa katika familia zaidi ya kujifunza mambo hayo kupitia katika TV, senema au miziki. Wanaume waliopitia malezi ya aina hii huchelewa sana kuoa kwani huyaangalia maisha ya ndoa kwa namna ya kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi kinyumba na wanawake kwa ajili ya kutaka kujifunza namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa na ndio sababu huchukua muda mrefu kufanya maamuzi. Na mara nyingi huishia kubadilisha wanawake kutokana na kutokuwa na uhakika wa kile wanachokitafuta.

Mgogoro wa kiuchumi: Kuna kundi kubwa la vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na kipato. Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume atakayependa kujiingiza kwenye ndoa wakati hana kazi au hana uhakika na kipato chake. Na hiyo ni kutokana na wanawake wengi siku hizi kuonekana kujali zaidi wanaume wenye uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake ya kebehi dhidi ya wanaume wasio na ajira au kipato, kama vile “mwanaume suruale” ina mchango mkubwa sana katika kuwafanya wanaume kukwepa kuoa iwapo hawana ajira au hawana uhakika na kipato chao.



Wanawake wengi kuwa na kiwango cha elimu ya juu: Siku hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya juu kwa juhudi kubwa. Idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi tofauti na ilivyokuwa zamani. Na hiyo ni kutokana na wazazi wengi kubadili mtazamo wao juu ya mtoto wa kike. Zamani mtoto wa kike alichukuliwa kama kitega uchumi. Kwa maeneo ya vijijini na katika familia masikini, watoto wa kike walikuwa wanatazamwa kama, ‘biashara ya kesho’ ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ilikuwa ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Lakini tofauti na zamani siku hizi hata kule vijijini kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa kumsomesha mtoto wa kike hadi elimu ya juu. Kutokana na mwamko huo wanawake wengi wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee la kuepukana na mfumo dume. Mwanamke gani atakubali kunyanyaswa na mwanaume akiwa na elimu yake na labda pia akiwa na kazi yake yenye mshahara na marupurupu ya kutosha, naamini watakuwa ni wachache sana ambao hawajiamini au waliathiriwa na malezi. Kwa upande wa wanaume nao, wamejikuta wakiwaogopa wanawake hawa wenye elimu ya juu kwa hofu ya kuzidiwa kipato na labda kukosa sauti kama mwanaume na hiyo inatokana na ego 
tu. 

Wanaume huwaona wanawake kama tishio wanapokuwa na mafanikio makubwa kifedha: Inaweza kutokea mwanaume anaweza kuwa na uhusiano na mwanamke ambaye labda tu nisema ni mbangaizaji. Wakati huo anaweza kuahidi kufunga ndoa na mwanamke huyo, lakini iwapo itatokea mwanamke huyo akapata mafanikio kibiashara na kuinuka kifedha. Kama mwanamke asipokuwa makini anaweza kusababisha mwanaume huyo akaingia mitini. Sababu kubwa hapo inaweza kuwa ni hofu ya kuogopa kuongozwa na mwanamke. Kumbuka kwamba mfumo dume bado umetawala vichwani mwa wanaume wengi kutokana na malezi. Mwanaume asiyejiamini ni vigumu sana kwake kuoa mwanamke aliyemzidi kipato. Kwa sababu akifanyiwa jambo dogo tu, inakuwa kama ametoneshwa. Atahisi kutaka kutawaliwa na mwanamke huyo. Jambo ambalo wanawake wanatakiwa kulifahamu ni kwamba kila mwanaume anataka kutambuliwa na kuheshimiwa kama shujaa kabla ya kumfuata msichana. Iwapo utakuwa umesimama iwe ni kifedha au kielimu pale unapotafuta kupata mwenza, inabidi ujishushe sana la sivyo utadoda.


Wanaume wengi siku hizi wana hofu ya majukumu, hasa ya kulea watoto: Kutokana na malezi yao au kile wanachokijua kuhusu watoto, baadhi ya vijana huamini kwamba, kulea watoto ni jambo gumu sana. Lakini wengine wanaamini kwamba, hata mke anapaswa kulelewa kama ilivyo kwa mtoto. Hivyo wanaamua kutafuta kwanza uwezo ambao haupatikani kiurahisi. Kuna wengine, ambao wamefundishwa au kuelekezwa na mila na desturi zao kwamba, kabla hawajaoa, ni lazima wawe na nyumba kwanza, tena kwao. Kwa hiyo, hawa hadi waje wapate uwezo wa fedha wanakuwa wameshachelewa.

Kuna baadhi ya wanaume, maisha bila ya ndoa wanayaona kuwa ndiyo bora kuliko yale ya ndoa: Kuna baadhi ya wanawake hujirahisisha sana kwa wanaume. Siku hizi ni jambo la kawaida sana kukuta mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa, wenyewe wanaita Trial Marriage. Na hapo ndipo unapokuta wanaume hawaoni tena umuhimu wa kuoa. Sasa kama mwanamke anaweza tu kuishi na mwanaume bila ya ndoa na mwanaume huyo akapata huduma zote kutoka kwa mwanamke huyo, unadhani ni kitu gani kitamvuta kufunga ndoa. Jambo lingine ni ile dhana kwamba maana ya ndoa ni tendo la ndoa. Siku hizi wanaume wengi wamejikuta wakiwa hawahitaji tena kuoa kwa sababu tendo hilo linapatikana kiurahisi tofauti na zamani. Siku hizi inawezekana kabisa kumtongoza binti leo na kupata tendo siku hiyo hiyo….. Na hapa siwazungumzii makahaba. Nawazungumzia mabinti zetu ambao wengine ukiwaona ni watu wa kuheshimiwa ukiwaangalia kwa nje lakini kwa ndani hawana lolote, vijana wa siku hizi wenyewe huwaita maharage ya Mbeya.

Kuna sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wanaume siku hizi kujivuta sana katika kufanya maamuzi ya kutafuta mwenza. Lakini hizo chache nilizozitaja zina mchango mkubwa.

UHUSIANO UNAPOVUNJIKA, WANAWAKE NDIYO HUUMIA ZAIDI....!


Kwa kuangalia idadi ya watu wanaoathirika kufuatia kuvunjika kwa uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume mtu atagundua kwamba wanawake ndiyo ambao hupatwa na athari kubwa zaidi. Kwa mfano ukichukua watu ishirini, wanawake kumi ambao wameachwa na wapenzi wao na wanaume kumi ambao nao wameachwa pia na wapenzi wao, utagundua kwamba, wakati ni wanaume watatu tu kati ya hao kumi ndio watakaosumbuliwa sana na na hali hiyo, kwa wanawake idadi itakuwa ni saba kati ya hao kumi. 


Watu wengi wanaweza kukimbilia kwenye kusema hali hiyo inatokana na utegemezi wa wanawake kwa wanaume. Hii ikiwa na maana kwamba, wanaathirika zaidi kwa sababu, kwa kuachwa ina maana pia kwamba hawataweza tena kupata mahitaji ambayo walikuwa wanapewa na wanaume hao. Dhana kama hii inaweza kuwa na ukweli fulani, lakini hali halisi inakataa. Kuna wanawake ambao wana uwezo mkubwa nap pengine ndiyo wanaowalisha na kuwavisha wanaume, lakini wanapoachwa na wanaume hao huathirika sana. 

Wanawake wa aina hii inadaiwa kwamba huathirika zaidi kuliko wale walio tegemezi. Kuathirika huku kwa ziada huhusishwa kwa kiasi kikubwa na ukweli kwamba wanaume ni watu wa kutoa ili kupalilia penzi, lakini hapa badala ya kutoa wanapewa na bado wanaondoka. Hili huwatanza wanawake wa aina hii. Lakini sababu ambayo huenda wengi wetu tulikuwa hatuijui kuhusiana na suala hili la wanawake kuathirika zaidi baada ya kuvunjika kwa penzi au kuachwa ni ‘ndoto.’ Kimaumbile wanawake huota zaidi ndoto za mchana au hufikiria zaidi kuhusu maisha yao ya kimapenzi yatakavyokuwa ukilinganisha na wanaume. Siyo kufikiria tu, bali hufikiria kwa njia inayoonyesha kuwa maisha hayo yatakuwa kama peponi.



Wanawake, wakiwa bado wasichana (baada ya kuvunja ungo) huanza kufikiria na kupiga picha jinsi busu lao la kwanza litakavyokuwa, mtu ambaye watabusiana awali. Hufikiria pia kuhusu wapenzi wao wa awali watakavyokuwana jinsi itakavyokuwa watakaposhiriki nao tendo kwa mara ya kwanza na huwa wanapiga picha ya jinsi siku yao ya harusi itakavyokuwa na watu watakaowaona. Katika kupiga picha huko huwa wanafikiria namna ambavyo mambo hayo yote yatakavyoenda vizuri bila doa, huwa wanajiona wakiwa wamefanikiwa katika hatua zote na hatimaye kuishi kwa raha mustarehe milele na watakaokuwa wapenzi wao. Kwa upande wa wanaume hakuna ndoto za aina hii na hata kama zipo ni kwa wachache sana, wakati kwa wanawake ni kama sehemu ya makuzi kwao. 


Kwa hali hiyo, ukiacha mazingira wanamokulia wanawake, kwa sehemu kubwa hukua wakiwa na hizo ndoto zao, ambazo kwao siyo ndoto bali ukweli. Wanapokuja kwenye ukweli wa uhusiano hugundua kwamba busu la awali siyo kama walivyotegemea liwe, mpenzi wa awali siyo kama walivyomtegemea awe na wala maisha ya ndoa siyo matamu kama walivyokuwa wameota. Kwa kuwa hawakujiandaa wala kutegemea mazingira magumu ya uhusiano, hawakuwa wakiota kuhusu ugumu wa uhusiano bali wororo, wanapokutana na masuala ya kuvunja moyo kama kuachwa hubabaika sana. Kwa kuwa akilini mwao walikuwa na picha ya mafanikio katka uhusiano, kushindwa kwa uhusiano, huwafanya wajione kwamba, wao ndiyo wakosaji, wameshindwa kulinda uhusiano ambao katika ndoto zao waliamini kwamba ni mzuri na usio na doa 


Ukiangalia kwa makini katika uhusiano, wanawake ndio wanaojitahidi sana kulinda uhusiano usivunjike, wao ndiyo wavumilivu zaidi, ndiyo ambao hujitahidi kuyarudisha mambo yaende sawa pale yanapokwenda kombo hata kama kufanya hivyo kunawagharimu. Yote hii ni juhudi yao ya kutaka kuishi kwa kadiri ndoto zao za kabla zilivyowaonyesha, kwamba uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume ni mtamu, mororo na usio na chembe ya doa……

No comments:

Post a Comment