Timu ya Toto Afrikan ya jijini hapa inatarajia
kujipima ubavu dhidi ya mabingwa wa ligi kuu ya Uganda Viper FC katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa
kwenye dimba la CCM Kirumba leo.
Mabingwa hao kutoka Uganda, Viper wanashuka dimbani
baada ya kuilaza Mbeya city 4-1 jijini Dar es Salaam, huku Toto wakiwa
wamepoteza dhidi ya Stand United 1-0.
Akizungumza na waandishi wa habari, kaimu mwenyekiti
wa Toto Afrikan Kenneth Petro alisema kuwa, mchezo huo ni wa kimataifa na wanaamini kuwa ni kipimo sahihi kwa Toto.
“Toto ni timu kubwa na lengo la usajili huu ni
kuipandisha timu ligi kuu lakini pia kucheza soka kwa kiwango cha kimataifa ili
tutakapokuwa mabingwa wa Tanzania basi tuweze kuwakilisha vyema”alisema dkt.kenneth
Toto afrikan ambayo inajivunia usajili wake kwa
msimu huu, inatarajia kuonyesha mashabiki kuwa usajili waliofanya ni sahihi na
kuwahakikishia kuwa watapanda ligi kuu msimu ujao.
Huku akihakikishia wadau wa soka jijini hapa, kocha
mkuu wa kikosi hicho ambaye ni baba mzazi wa mchezaji Jerry Tegete, John Tegete
alisema kuwa, kikosi chake kipo fiti na ushindi si jambo la kuuliza.
“Tulipocheza na Stand United tulikuwa tumetoka
kwenye mazoezi magumu lakini pia tulikuwa tumechoka na safari ila kwasasa timu
ipo kambini na wanafanya mazoezi mepesi yanayoenda na mchezo wenyewe”alisema
kocha Tegete.
Pia Makamu mwenyekiti alisema, timu ya Viper inashiriki Ligi kuu nchini
Uganda na kwamba msimu uliopita ilishika nafasi ya kwanza katika msimamo wa
ligi kuu ya nchini humo, na baada ya mchezo huo wataelekea mkoani Shinyanga.
Kiingilio katika mchezo huo ni Sh3,000 kwa Sh5,000
jukwaa kuu.
No comments:
Post a Comment