Maji moto ya
Mutagata kugharimu mil.22 kuweza kutoa huduma bora, Kagera
Jumla ya shilingi za kitanzania milioni
22, 935, 250 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya kulala wageni na vyoo
kwa wagonjwa na watalii wanaokwenda katika msitu wa hifadhi ya majimoto katika
kijiji cha Rwabigaga wilayani Kyerwa mkoani kagera.
Msitu wa Hifadhi ya Maji Moto (Mutagata
Hot Spring catchment forest) ni moja ya kivutio kikubwa katika wilaya ya
Kyerwa, unaopatikana katika kijiji cha Rwabigaga eneo la Mutagata, kata ya
Kamuli, tarafa ya Kituntu/Mabira.
Akizungumzia ujenzi huo, mwenyekiti wa
kijiji cha Rwabigaga Froni Nestory alisema kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya
kubaini kuwa na uharibifu wa mazingira lakini pia utasaidia katika kuongeza
pato la serikali ya kijiji hicho.
“Tumeamua kujenga nyumba ya vyumba vinne
na vyoo vyenye mashimo mawili ili wageni kutoka nje ya kata ya Kamuli
watakapohitaji huduma hapa watalipia shilingi 5,000 kwa kila mmoja kwa lengo la
kukuza pato la kijiji pia na gharama za utunzaji wa eneo hili la kihistoria,”
alisema.
“Ujenzi huu ni nguvu za wananchi ambao
kila mmoja alichangia shilingi 2,000 huku shirika la Hifadhi Mazingira
Yakutunze (HIMAYA) ambao walichangia kiasi cha shilingi 935,250 kwaajili ya
ujenzi wa vyoo ili kuepuka hadha ya kujisaidia hovyo hasa msimu wa mvua,
serikali ya kijiji ikichangia kiwanja na shilingi za kitanzania milioni 22
kwaajili ya ujenzi wa nyumba ya kulala wageni,” alisisitiza Nestory.
Aliongeza kuwa, “baada ya ujenzi huo
kukamilika tuta tangaza tenda ya kulisha chakula eneo hili; hadi sasa
hatujapata msaada wowote kutoka Halmashauri licha ya viongozi mbalimbali
kuhudhuria wakiwemo wakuu wanne kupanda miti ya asili eneo hili na pia
kupelekea mapendekezo yetu katika ngazi ya wilaya lakini hakuna jibu lolote
hadi sasa”.
Msitu huo ni umbali wa kilomita 70
kutoka makao makuu ya wilaya; Msitu huu ni wa kijani kibichi muda wote
uliotanda miti ya Misambya (Markhamia Lutea) na miti mingine ambayo majina yake
hayafahamiki vyema.
Katika msitu huu vipo vyanzo vinne vya
maji moto, vyanzo hivi ni; Kasiyoza ambacho ni chanzo kikubwa cha maji moto
katika eneo hili ambalo maji yake ni nyuzi joto 60-90; Chabakazi ambalo ni eneo
dogo linalotoa maji ya moto yenye nyuzi joto 40-60; Katagata kake hili ni eneo
jingine ambalo maji yake ya moto yana nyuzi joto 30-50 na Chandagala chenye
maji ya baridi.
Katika kutafuta ushuhuda wa tiba hii
inayoaminika kwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita kuwa inatibu na wagonjwa kadhaa
kuthibitishwa kupona, nilikutana na mama mmoja aliyekuwepo eneo hilo kwa
matibabu.
“Nashukuru sana kuletwa hapa maana
nimeugua hii miguu kwa miaka sita bila kutembea leo hii kama unavyoniona
naendelea vizuri kwani naweza kutembea, na nina siku tatu toka nimefika hapa,”
alisema Kotilda Marco (35) ambaye alikuwa amepelekwa eneo hilo kwa ajili ya
kupata tiba ya miguu,” Bi Kotilda alieleza.
“Maji haya ni tiba yenye kuponya kwani
leo unaniona hivi ila nimeletwa hapa sikuwa naweza kutembea hata kwenda
kujisaidia nilikuwa napelekwa, lakini sasa naweza kwenda hata pale juu kuoga
mwenyewe na kurudi ama kweli Mutagata ni ponyo kwetu,” aliongeza mama huyo.
“Historia inaonyesha kwamba chem chem
hii ilitumiwa na machifu kuoga; Chifu Rumanyika alitembelea eneo hili na
kuliwekea Baraka, akaitukuza chem chem hii na kulitangaza eneo hili kuwa sehemu
takatifu na kuanzia wakati huo, maji hayo hutumika kwa ajili ya tiba ya
magonjwa ya ngozi kama vile upele na mapunye, kifua, uvimbe wa miguu, magoti
n.k.
”
Boniface Mshonga ambaye ni
Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha
Mutagata.
“ Licha ya chanzo hiki kusaidia katika
kuponya lakini ni moja ya utalii ambao kama serikali itaweza kukitumia vyema;
ila inavyoonekana chanzo hiki kinaweza kuharibiwa na wakazi wa eneo hili ambao
wamekuwa wakiyatumia maji haya kwa kufulia na kunyweshea mifugo huku misitu hii
wakitumia katika matumizi ya nyumbani,” alisisitiza.
Hata hivyo, ili kupata historia zaidi
nilimtafuta mzee maarufu mwenye umri mkubwa ili kuweza kunijuza hasa kuhusu
chanzo cha maji haya.
“Aliyeleta maji haya ni shangazi kutoka
katika utemi katika kabila la Buganda, wakati alipokuwa akitokea Rwanda
kuelekea Uganda na alipofika hapa alikuwa amevimba miguu na amechoka sana yeye
pamoja na watumishi wake ndipo alitamka kuwa ee Mungu ungenisaidia maji ya
kukanda hii miguu ili niweze kuendelea na safari na kasha maji hayo yakatokea
na kuyabariki kuendelea kutumika hadi leo,” alisema mzee Busisi kayombagani
(101) ambaye ni mzaliwa wa eneo hilo.
“Baada ya kuyaacha maji hayo kwa
kuendelea na safari ndipo yalibaki yakiangaliwa na kabila la Wahinda chini ya mtemi(chief)
Rumanyika hadi ukoo huo ulivyoamua kuhama eneo hilo na mmiliki kufariki, eneo
hilo likamilikiwa na kabila la ukoo wa Muhunga ambao walikuwa wakimuita mtemi
Rumanyika babu kutokana na kuozana hadi leo,” alisisitiza.
Na kuongeza kuwa,“kwasasa mila na
desturi za eneo hilo zimebadilika kwani zamani hakuruhusiwa mwanamke ambaye
yupo kwenye hedhi wala mtoto ambaye hajaota meno wala kutenda tendo la ndoa
eneo hilo na alipokuwa akikosea mmoja wapo lazima madhara yatokee wakati ule
ule, lakini leo unaona watu wanaoga katika maji hayo na watoto pia wanaoga hadi
mifugo inanyweshwa hapo na hii yote ni kutokana na watu wa kabila linalomiliki
kushindwa kufanya matambiko ambayo yalifanywa hapo awali kama vile kuchinja,
ng’ombe na kunywea katika eneo maaalum pombe ya kienyeji”.
Tunapozungumzia historia ya watu wa
mahali fulani hatuna budi kuzungumzia Jiografia ya sehemu husika, hali ya hewa
na mazingira, wakazi wake, uoto wa asili, utamaduni wao, utawala, mawasialiano
na uchumi.
Lengo la kutafuta na kuifahamu vyema
historia ya watu wa Kyerwa ni la msingi sana kwa kuandaa mazingira ya watu
mbalimbali ili waweze kuielewa vyema historia ya Kyerwa, kukusanya
na kuzihifadhi zana na kumbukumbu za kimila na jadi ambazo katika siku za
karibuni zinaelekea kuanza kupotea.
Makala hii inachambua kwa kina historia
ya msitu wa hifadhi ya maji moto ambao kwa asili unapatikana Wilaya ya Kyerwa
Mkoani Kagera.
Kwa upande wake mtunza eneo hili ambaye
anadaiwa kutoka katika ukoo wa Muhunga ambapo mtemi Rumanyika alioa huko,
hakusita kuelezea kile anacho kifahamu katika eneo hilo.
“Kama unavyofahamu mtemi Rumanyika
alifanya mambo mengi ambayo hadi leo yamebaki ni historia isiyopotea, hivyo
katika kumuenzi ndio maana unaona eneo hili linaendelea kuwepo na vitu vyake
vya asili ambavyo nitakwenda kukuonyesha,” alisema Angelo Mathias mtunza eneo
hilo.
“Kama unavyoona jiwe hili la kukalia
ndipo alipokaa Kanyabugondo shangazi wa utemi wa Buganda na mpaka leo hutumika
kukalia na kuogea kwa wagonjwa wanaofika eneo hili na hapa pembeni sehemu ya
kuweka sabuni au marashi kwani machifu walitumia kuwekea sabuni wakati wa kuoga
na palitengenezwa kwa mikono na malkia huyo; pia hili bao lilitengenezwa kwa
mikono, na chifu Rumanyika na wageni wake walitumia wakati wa kupumziko lakini
eneo hili lilitumika wakati wa tambiko na hapa ni eneo la kutupa mawe au pesa
kwa wanaofika kupata huduma hapa,” aliongeza.
Mbali na kivuto hicho cha maji moto pia
katika wilaya ya Kyerwa na Karagwe kuna mapori manne ya Akiba za
wanyamapori ambayo ni Rumanyika Orugundu, Kimisi, Ibanda na Burigi.
Mbuga hizi zina wanyama wengi kama vile
pofu, nyemera, mamba, viboko, twiga, simba, kuro, nyati, tembo na ndege wa aina
mbalimbali.
Mapori haya ya Akiba mbali na kuwa kivutio kwa watalii na wananchi
wanaopenda kuangalia wanyamapori, mito na mabonde; vile vile hutumika kwa
shughuli za uwindaji wa kitalii.
Wanyambo ambao ndio wenyeji wa eneo hili
ni kabila lilokuwa miongoni mwa makabila makubwa na yenye nguvu za kivita na
kiuchumi.
Utawala wa kabila hili ulikuwa wa
kifalme ulioongozwa na wafalme “Abakama” 14 kwa nyakati tofauti huku watu wake
ni wakulima na wafugaji.
Kabila la Wanyambo linapatikana katika
Wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera.
Inaaminika kuwa asili ya jina la kabila hili
ni eneo la Maziwa Makuu na jina la kabila hilo limetokana na aina moja wapo ya
ndizi inayofahamika kwa jina la Enyambo.
Aidha neno nyambo linamaanisha mtu au
kitu au mmea asilia pia yupo ng’ombe wa asili wilayani Karagwe ambaye
anajulikana kwa jina la Enyambo linalofahamika katika nchi za Uganda na Rwanda.
Himaya ya mfalme wa Karagwe ilikuwa
ndiyo utawala mkubwa katika maeneo ya maziwa makuu kwa miaka kama 500 na
Bweranyange Mji Mkuu wa Mfalme wa Karagwe ndipo alikaa mfalme Ruhinda wa
kwanza, mwanzilishi wa himaya za Kihinda.
Ruhinda alitawala eneo lote la Karagwe,
Ankole, Kihanja, Ihangiro Biharamulo Bushubi, Bugufi Kaskazini, kipakana na
Bunyoro na mto Mwiruzi Kusini ya Biharamulo na Mkoa wa Kigoma.
Licha ya kutofahamika katika Tanzania ya
leo sambamba na kupanda na kushuka kwa umaarufu wa kabila hilo.
Himaya ya mfalme
wa Karagwe hiyo ilitukuka na kuandikwa kwenye magazeti ya ulimwengu wakati wa
wavumbuzi hususani Uingereza zaidi ya miaka 1600.
Jina “ Karagwe “ ambalo limezaa wilaya
mpya ya Kyerwa kutokana na simulizi za wazee wetu mbali mbali na watafiti wa
historia ya Karagwe kama (Katoke 1975;162) inaelezwa kwamba jina
hili linatokana na kilima kinachopatikana Kusini Magharibi ya Makao makuu ya
wilaya ya Karagwe, kwenye kijiji cha Kandegesho, kata ya Nyakakika
ambacho mtawala (Omukama) wa kwanza alifanya kafara ya kwanza.
Na kwamba kumbukumbu hii ya “Karagwe ka
Nono “inatokana na ukweli kuwa Nono alikuwa mtawala wa mwisho wa wenyeji asilia
wa Karagwe kabla ya kuondolewa madarakani na Omukama Ruhinda mtoto wa Wamara.
Inasemekana kwamba Nono son of Marija
alikabidhi madaraka yake bila ya misukosuko wala mapigano ya aina yoyote kwa
ajili ya kuokoa watu wake waliokuwa wanakabiliwa na wimbi la njaa.
Birigitta Farelius 2008 katika utafiti
wake anasema “ Popote unapokuta ng’ombe machungani katika Afrika ya Mashariki
macho huvutiwa sana na ndege weupe (white cow herons) wajulikanao kama Nyange
Nyange , nao watu wa Karagwe huwaita Enyange, wakifuatana na ng’ombe huku kazi
yao kubwa husaidia kudonoa kupe na wadudu wanashambulia mifugo.
Makao makuu ya Omukama Rumanyika wa
Karagwe yalikuwa katikati ya makundi ya wafugaji na kulikuwepo na ndege hawa
wengi na hivyo kupewa jina la Bweranyange kutokana na ndege hawa kupenda
kutanda eneo hili muda wote
Na hili linathibitishwa na simulizi za
wenyeji wa eneo hili ambao wengi walikuwa wafugaji, na sisi pia tunalazimka
kukubaliana na matokeo ya utafiti huu unaonyesha chimbuko la jina la
Bweranyange wakiwa na maana sehemu safi na nyeupe (makao makuu ya mtawala wao)
kutokana na umaarufu wa ndege hawa.
Ni kutokana na ukweli huu wenyeji
walitunga wimbo maarufu wa kumsifia mtawala wao, na kwa mtawala halisi na
makini kama alivyokuwa Omukama Rumanyika alitakiwa kuwa na roho nyeupe ya
upendo kwa watu wake na wimbo huu ulikuwa unaimbwa popote pale alipotembelea na
kulala.
Wimbo huu uliwaasa na kuwaonya wananchi
kuwa wasikivu, wastaarabu, wenye kufuata kanuni, sheria na kutokuwa wasumbufu
kwa mgeni wao aliyewatembelea.
“Mtayomba mwalirwa enyange ……….
Mtayomba
…………………………….
Ne enyange ti nyange …………………
N’omwana ‘womuntu ……………..
Mtayomba
…………………………..
Leba no omwana wo omuntu ……….
Mtayomba ………………………….” Hii ni sehemu ya
wimbo huo.
Taarifa za Utafiti huu unashabihiana kwa
karibu sana na ule wa Bwana HALLEY katika kitabu chake cha “An African Survey “
ukurasa 23/24 “ akielezea kwamba kaskazini magharibi mwa ziwa Victoria ‘’ Watu
wa makabila ya Waganda, Wanyankole, Watoro, Wanyoro na makabila manane ya
wilaya ya Bukoba katika Tanganyika na Ruanda (Nchi ya udhamini ya ubeligiji) ni
mchanganyiko wa makabila ya wenyeji wakulima wabantu na makabila ya wafugaji wa
kihima toka kaskazini ambao yanasadikiwa kwamba yalizishambulia nchi hizo zama
za miaka mia tatu iliyopita na kuwashinda wenyeji wake.
KUHUSU BIASHARA
Mwishoni mwa karne ya 18 na mwanzoni mwa
karne ya 19, habari za kushamili
kwa Karagwe kutokana na biashara zilikuwa
zimesambaa sehemu mbalimbali za nchi ya Tanganyika pamoja na nchi za
jirani za Rwanda, Kongo, Uganda, Burundi na hata nchi za Falme za Kiarabu.
Wakati huo Karagwe ilikuwa imekwisha tembelewa
na wajasiliamali toka Unyamwezini na Usumbwa ambao walileta chumvi toka Uvinza
na chuma toka Katanga (nchini Kongo).
Hili linathibitishwa na msemo wa
kinyambo wa muda mrefu unaosema “Omwonyo ngunula, chonka Omushumbwa nanunka”kwa
kiswahili maana yake ni kwamba chumvi yao ni tamu pamoja na kwamba wachuuzi
wenyewe wanatoa harufu mbaya ya jasho kutokana na safari yao ndefu.
Inaaminika pia kwamba Wanyamwezi
walifika Karagwe wakiwa watu wa kwanza kufanya biashara na kwamba walileta
chumvi, visu, pilipili, na matunda kama vile maembe, machungwa na mtama
kabla ya Waarabu kuingia ambao walijenga Kituo chao maeneo ya Kafuro na
Kitengule.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wakati
Omukama Rumanyika Orushongo anaingia madarakani, Karagwe ilikuwa tayari imekua
kiuchumi kiasi ambacho wafanyabishara toka maeneo ya mbali walikuwa wameanza
kuingia Karagwe wakifanya biashara ya meno ya tembo, mazao ya chuma (Iron products)kama
vile visu, majembe na vitu vingine wakibadilishana na bidhaa waliyoleta toka
maeneo waliyotoka.
Shughuli za Kisiasa, biashara na watu wa
mbali (Tabora na Pwani) ilianzisha na kujenga mahusiano mazuri na watawala (Abakama)
wa Karagwe, kiasi kwamba Omukama Rumanyika I wakati huo alilazimika kumteua
msadidizi wake (Kiyango kya Mpiga Ifumula Bikungu) kuwa Balozi wake katika
tawala za jirani zake ambaye wakati huo alikuwa akisafiri kati ya Bweranyange,
Buganda, Bunyoro na Tabora.
Kazi kubwa ya mteule Kiyango kya Mpiga
Ifumula Bikungu ambaye unaweza kumuita Kama balozi ilikuwa ni kufanya mawasiliano
na kuimarisha kati ya Mtemi Rumanyika na watawala wa sehemu
hizo.
Balozi huyu alionekana kupata sifa
nyingi za utendaji kazi, sifa ambayo ilitolewa wazi wazi na wageni kama
Captain John Hanings Speke na Grant (katika kitabu chake kiitwacho “The
jouney of discovery of River Nile” ) walipozuru Karagwe, ilikuwa ni kupitia
kwake wageni hawa waliweza kupokelewa na watawala ikiwa ni pamoja na Omukama
Rumanyika bila matatizo yeyote.
Haya yanathibitishwa na mzee wetu
marehemu Profesor Katoke (1975;55) ambaye aliandika
“Ikumbukwe kuwa Speke na Grant walipata upinzani mkubwa katika sehemu
zingine za Kigoma na Tabora ambapo waliingia bila kuwasiliana na Kiyango,
waliweza kuzuiliwa kwa muda na wakati mwingine kutozwa ushuru mkubwa na
watawala wa maeneo hayo wakiwa safarini kuelekea Karagwe”, hii
inathibitisha umuhimu wa Balozi huyo Kiyango cha Mpiga Rufumura Bikungu.
Karagwe ilitumika kama njia pekee ya
kufikia utawala wa Buganda kwa wageni toka Pwani na Zanzibar.
Kati ya Novemba 1861 na Februari 1862
John Hannington Speke na James Grant walikaa miezi mitatu Kafuro jirani na
Bweranyange na wakaandika kwa kirefu juu ya mila na desturi za Karagwe chini ya
mfalme Rumanyika Orugundu Rzinga Mchuchu wa Nkwanzi ambalo ni jina la utani
lenye maana ya shujaa mfuga nywele ndefu mwana wa Nkwanzi.
Na kwamba, kwa hivi sasa kuna hifadhi ya
wanyama ya rumanyika Orugundu kuenzi mtawala huyo ambayo kwa mashariki yake
katika kijiji cha Ibamba kunapatikana mto wenye maji moto ya Mutagata”anasema
Tuluhungwa.
Historia ya kabila hili ilifahamika
ukanda wote wa Ziwa Victoria Magharibi pamoja na nchi za Rwanda na Burundi
Kutokana na uhunzi wa mapambo mengi ya kifalme yalitengenezwa na kuhifadhiwa
kwenye ngome ya mfalme.
Mapambo hayo yalipendwa na mengine
yalichukuliwa na Wajerumani, walipewa zawadi na Omukama Rumanyika.
Ni kabila lililoheshimika na wanyambo
walijivunia Unyambo wao hali iliyoibua misemo kama, Ndyu Munyambo akala
nakalenje, Omunyambo agamba echabweine.
Kabila la wanyambo ni miongoni mwa
makabila makubwa Mkoani Kagera mengine ni Wanyambo wenyewe, wasubi, washubi,
wahangaza, wazinga na wahaya.
KUPOTEZA UTAJIRI
Karagwe ilianza kupoteza utajiri wake
katika miaka ya 1880 na 1890 ambapo wakoloni wa kijerumani walikuwa wakishidana
kuligawana bara la Afrika huko Berlin 1884 na baadaye wakati Zanzibar na
Buganda zilikuwa tawala zinazolindwa na mfamle wa Uingereza.
Karagwe iliangukiwa na nuksi ambazo
zilifika tawala nyingine zote kubwa katika historia kama za Alexander mkubwa
utawala wa Kirumi.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo
vilikuwa vimeanza wakati Speke na Grant wakiwa Karagwe Novemba 1861 mpaka
Desemba 1862 Matokeo yake ilikuwa kupungua kwa amani na kuihama Karagwe upande
ulioshindwa na kupunguza wingi wa watu.
Pili ugunduzi wa njia fupi toka Mombasa
kwenda Uganda kulitoa Karagwe kwenye njia Kuu ya biashara ya kimataifa na
kupunguza umaarufu wake.
Magonjwa ya mifugo kama ng’ombe sotoka
ilishambulia mifugo ya wakazi wa karagwe katika kipindi hiki na kupunguza
utajiri wa Karagwe pia wakoloni walikuwa hawavutiwi na nchi maskini.
Karagwe iliathirika kisiasa na kiutawala
baada ya wafalme wake wengi kufa wakiwa wadogo bila kuacha warithi
walioishafikia umri wa kutawala, ikalazimu kutawala kwa kutumia viongozi wa
muda kama vile Kakoko waliotawala kwa ukatili na kuharibu himaya.
Pia Karagwe haikupewa kipaumbele katika mipango ya wakoloni
wa Kijerumani kulifanya Wamisionari kutovutiwa kuweka vituo vyao Karagwe.
Wamisionari wa Kikatoliki walianzisha
vituo vyao Kashozi 1892, Bunena 1905, Kagondo na Rubya 1904, Katoke Biharamulo
na kuanzisha shule sehemu zote hizo.
Misheni ya kwanza Karagwe ilianzishwa
1934 baada ya miaka 40 baada ya kumpata Padri wa kwanza mwafrika wa kwanza
Oscar aliyepadrishwa Bukoba 1917 ambaye wa kwanza Karagwe Padri Rwakiboine
alipandrishwa 1943 miaka 26 baadaye na shule na hospitali zilifata misheni.
Kwasasa Karagwe na Kyerwa imekumbwa na
tatizo la kukosekana kwa mvua hali inayopelekea mazao mengi kukauka, hivyo
wakazi hao kukumbuka utawala wa kichifu ambao haukuwahi kuonekana kwa tatizo
hili la kukosekana mvua hadi sasa.
No comments:
Post a Comment