Friday, July 18, 2014

POLISI, WAANDISHI WA HABARI KUPATIWA MAFUNZO YA MILIPUKO


Kutokana na kuongeza kwa milipuko ya mabomu nchini ambayo imekuwa ikileta madhara hasa kwa waandishi wa habari na askari polisi, chuo cha Dar es Salaam cha uandishi wa habari na mawasiliano ya umma (DIJM) kupitia tawi lake la jijini Mwanza, kinatarajia kutoa mafunzo maalum kuanzia August 11 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, mkurugenzi wa chuo hicho Jackson Wambele alisema kuwa, lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuwaelimisha polisi na waandishi wa habari ambao kwa pamoja wanashiriki katika milipuko.

“Unajua milipuko ya mabomu hapa nchini kwetu ni uharifu mpya na waandaaji hutumia malighafi ambazo zinatumika katika uzalishaji, lengo ni kuwafundisha waandishi namna ya kuripoti katika eneo la tukio huku polisi wakitarajiwa kufundishwa kuzuia uharifu” alisema Wambele.

“kuna matukio mengi ambayo yamekuwa yakitumia milipuko kama vile Wizi, uvuvi, kuzuia ghasia, nk hivyo mafunzo  haya yataelekeza jinsi ya kukabiliana na changamoto za uharifu unaotokana na milipuko”alisisitiza.

Na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika na chuo hiki kimebaini kuwa kwa sasa nchi yetu imekuwa ikikumbwa na milipuko ya mara kwa mara ambayo imechangia watu wengi wakiwemo waandishi wa habari na polisi kupoteza maisha.

“Baadhi ya maeneo ya milipuko hiyo ni Mlipuko wa bomu Katika Ghala La Jeshi Gongo La Mboto Jijini Dar Es Salaam ambapo watu zaidi ya 25 walithibitishwa kuwa wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa vibaya, mlipuko wa bomu uliotokea katika mgahawa wa Traditional Indian Cusine, Gymkhana, Kanisani Olasiti, Mkutano Chadema Soweto, Usa River siku ya Mkesha wa mwaka mpya, Vama Restaurant na chupuchupu kulipua nyumbani kwa RC jijini Arusha” alimaliza.

Kwa upande wake inspector Henry kutoka kitengo cha upelelezi aliyemwakilisha kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema kuwa, suala la ulinzi ni changamoto hata kwa nchi zilizoendelea.

“Tunashukuru sana kwa kuona kuwa kuna wadau ambao wanaguswa na matukio haya na wapo tayri kutoa elimu kwa lengo la kuelimisha, nasi kama jeshi la polisi tunaahidi kutoa polisi watakaoshiriki katika mafunzo, vifaa vya mafunzo pamoja na wataalam watakaofundisha”alisema inspector Henry.

Naye Gereld Robert, akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari alisema kuwa, jinsi ya kuepuka milipuko kwa kushirikiana na polisi ni jambo muhimu na limekuja wakati muafaka.

“Sisi waandishi wa habari tunawashukuru sana kwa kuthamini mazingira ya waandishi wa habari wakati wa machafuko kwa ni hatari na hivi karibuni mwenzetu Daudi Mwangosi alipoteza maisha katika mazingira kama haya, hivyo tunaamini mafunzo hayo pamoja na umoja utaojengeka ni tunu kubwa”alisema Gerald mmiliki wa gazeti la Baruti.

Mbali na milipuko hiyo, hivi karibuni katika kanisa la kiinjili la kilitheri Tanzania (KKKT) la jijini Mwanza liliweza kuripotiwa kupatikana na mlipuko wa bomu la kienyeji na kufanikiwa kumjeruhi mtu mmoja.

No comments:

Post a Comment