Friday, July 18, 2014

Nafaka bingwa kombe la polisi jamii

Timu ya Nafaka Fc ya wilayani Misungwi mkoani Mwanza imejitwalia ubingwa katika mashindano ya polisi jamii kwa kuifunga Muungano Manawa fc kwa mikwaju ya penati 8-7, baada ya ushindi wa bao 1-1.
Mchezo huo wa fainali uliofanyika tarafa ya Misasi wilayani Misungwi, ulikuwa wa kuvutia hasa baada ya magolikipa wa timu zote mbili kuweza kufuta mikwaju mitatu ya penati kila mmoja huku kipa wa Muungano Manawa fc, Charles Simeo akiizamisha timu yake baada ya kukosa penati kwa kufutwa na kipa wa Nafaka fc Chila Abdallah.
Mashindano hayo ya polisi jamii ambayo yameanza mwaka 2013, yamekuwa yakidhaminiwa na inspector Majaliwa Ngaiza kwa kushirikiana na diwani wa Misasi Khaleed Mbitiaza, ambayo yanalenga kuwezesha jamii na wadau wengine kushiriki moja kwa moja katika kupanga mikakati na vipaumbele vya siku vya polisi wa eneo katika kubadilishana kwa ushirikiano wao katika juhudi za kuzuia na kupunguza uhalifu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi ambazo ni kikombe na Sh400,000 kwa timu ya Nafaka fc, Sh200,000 kwa Muungano Manawa fc na Inonelwa fc sh100,000; Inspector Ngaiza aliwataka vijana kuachana na vitendo vya uharifu.
“Tumeamua kuwashirikisha vijana hasa wavulana kwani uharifu mwingi unafanywa na vijana ndiyo maana tumeamua kuwaelimisha kupitia mashindano haya, tunaamini wataepuka vishawishi vya uharifu na watashiriki katika kudhibiti uharifu kupitia ulinzi shirikishi”alisema Ngaiza.
“Tumeanza mashindano haya mwaka 2013 katika eneo la Misasi, Ushiriki mkubwa wa jamii katika ulinzi wa polisi umeleta mafanikio makubwa kwa kupunguza uharifu na tunaelekea kuumaliza kabisa kama katiba inavyoeleza ambapo Ibara ya 146(2) (b) inaeleza polisi jamii kutoa huduma ambayo jamii inastahili; Hii ni muhimu hasa kutokana na hali ambapo Jeshi la Polisi linakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi na miundombinu”alisisitiza.
Na kuongeza kuwa, Katika jamii ya kidemokrasia, utekelezaji wa sheria ni wajibu wa pamoja kati ya vyombo vya wahimizaji sheria na wananchi kwa muktadha huu, inakubaliwa kwa jumla kuwa utaratibu wa kijamii wa udhibiti wa kijamii unatoa mchango mkubwa kuliko utaratibu rasmi wa polisi kwa msingi uliyozoeleka wa kuwa tayari kutenda na kutekeleza.
Michuano ya polisi jamii ilianza Juni 16 na kufikia tamati Julai 16 mwaka kwa kushirikisha timu 12, huku bingwa mtetezi Misasi Star akishindwa kutamba katika hatua ya mtoano.
Timu zilizoshiriki ni Misasi Star, Balimi fc, Isakamawe fc, Kasololo fc, Vijana Misasi fc, Ishokela fc, Mwanangwa fc, Kabale fc, Inonelwa fc, Seekee fc, Muungano Manawa fc na Nafaka fc.

No comments:

Post a Comment