Monday, October 20, 2014
EBOLA YAIPAGAWISHA MOROCCO, KUBWAGA MANYANGA UENYEJI AFCON 2
MOROCCO wanajiandaa kujitoa kama Wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2015, yaliyokuwa yafanyike Nchini kwao kuanzia Tarehe 17 Januari 2015 hadi Tarehe 8 Februari 2015 kwa hofu ya Ugonjwa wa Ebola ambao umeikumba Nchi kadhaa za Afrika Magharibi na kuua Watu zaidi ya 4,000.
Serikali ya Morocco iliipa CAF mambo matatu ya kuchagua ambayo ni wao kuwa Wenyeji wa Mashindano ya 2017, CAF waahirishe AFCON 2015 hadi 2016 ama wao wajitoe kabisa.
Lakini habari kutoka huko Nchini Morocco zimedai CAF imekataa mambo yote hayo matatu yaliyopendekezwa na Nchi hiyo na sasa wanatafakari kupeleka AFCON 2015 huko Afrika Kusini au Sudan ambao tayari wamesema wako tayari kuyaandaa Mashindano hayo.
Mbali ya Nchi hizo, inasemekana hata Egypt imesema iko tayari kuaandaa Mashindano hayo licha ya kuwepo muda mfupi mno.
Mwezi Desemba, Morocco pia itakuwa Mwenyeji wa Mashindano ya FIFA ya Kombe la Dunia kwa Klabu lakini hamna tamko lolote kuhusu michuano hiyo.
Ikiwa Morocco watajitoa rasmi kuwa Wenyeji wa AFCON 2015 ni wazi CAF itawachukulia hatua kali ambazo zitaathiri Timu yao ya Taifa na Klabu zao katika ushiriki wao Mashindano ya Kimataifa.
Hivi sasa AFCON 2015 ipo hatua ya Makundi ambayo itamalizika Novemba 19 ili kupata Nchi 15 zitakazojumuika na Morocco kucheza Fainali.
Mpaka Jana, wakati kila Kundi limebakisha Mechi mbili, ni Algeria pekee ambayo ndio imefuzu kucheza Fainali hizo baada ya kushinda Mechi zao zote nne za kwanza za Kundi B.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment