Tuesday, February 3, 2015




Bondia wa kulipwa nchini Tanzania, Francis Cheka, ambaye ni maarufu kwa jina la SMG, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kumpiga meneja waje wa baa yake , Bahati Kibanda.
Cheka alitiwa hatiani Julai 2 mwaka jana kwa kumpiga na kumsababishia maumivu makali Kibanda ambaye alikwenda hapo kudai fedha zake katika baa aliyokuwa anaifanyia kazi ijulikanayo kwa jina la Vijana Social Hall.
Cheka anayeshikilia mkanda wa WBF alipandishwa Kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, kwa shitaka hilo lililosomeka kuwa ni la shambulio la kudhuru mwili na kujeruhi.
Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya mkoa wa Morogoro Said Msuya alikubaliana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kuthibitisha shitaka hilo.
Cheka anadaiwa kutenda kosa hilo kwa Kabanda ambaye alikuwa ni Meneja wa baa yake ya Vijana Social iliyopo maeneo ya Sabasaba katika Manispaa ya Morogoro baada ya kudaiwa kutoridhishwa na mahesabu ya mauzo.
Hakimu Msuya alisema kuwa adhabu hiyo ni fundisho kwa mshitakiwa na watu wengine wanaotumia vibaya nguvu zao kwa watu wengine na anatakiwa kumlipa mlalamikaji fidia ya Sh milioni moja.
Pamoja na Cheka kupewa nafasi ya kujitetea, bondia huyo hakutoa maelezo yoyote na kuiachia mahakama hiyo kutoa adhabu inayostahili kwa bondia huyo aliyejizolea sifa kemkem katika ngumi za kulipwa nchini.
Hata hivyo, familia ya Cheka inampango wa kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.






No comments:

Post a Comment