Je, Toto inaweza kutimiza ndoto za kurudi ligi kuu
kwa staili hii?
Kikosi cha Toto katika Ligi daraja la kwanza
kilifanikiwa kushika nafasi ya tatu mbele ya Mwadui na Stand United katika
kundi C na kufanya stand kupanda ligi kuu kwa kuongoza, katika ligi daraja la
kwanza msimu uliopita.
Mbali na matokeo hayo mazuri yaliyochangiwa na
uchaguzi mpya wa klabu hiyo ambapo viongozi hao waliikuta timu hiyo ikiwa
katika nafasi ya pili kutoka mwisho katika msimamo wa kundi.
Maswali makubwa ya kujiuliza ni vipi viongozi hawa
wanaweza kuipandisha ligi kuu msimu huu, licha ya usajili waliofanya msimu huu.
Mgogoro mkubwa unaonekana kuikumba klabu ya soka ya
Toto Africans maarufu kwa jina la Wana-Kishamapanda inayoshiriki Ligi soka
daraja la kwanza Tanzania Bara, baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo,Omari Said
Mbalamwezi kuandika barua rasmi ya kujiuzulu nafasi hiyo Agosti mosi mwaka huu
Mbalamwezi amejiuzulu nafasi hiyo huku akieleza wazi
kwenye barua yake kuwa,ni kushindwa kuwajibika ipasavyo kwenye nafasi yake
kutokana na Makamu Mwenyekiti kutomshirikisha katika yale yanayoendelea kwenye
klabu hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jijini Mwanza, Makamu
mwenyekiti wa klabu hiyo, Ahmed Waziri Gao alisema kuwa, kujiuzulu kwa Mbalamwezi ni
kutokana na kuwa na majukumu mengi na bado wanajipanga kukaa katika kikao ili
kuijadili barua hiyo.
“Tunajiandaa kukutana ili kuijadili hatma ya
kiongozi huyo ambaye kwa barua tuliyoipata sisi amedai kuwa anajiuzulu kutokana
na kuwa na majukumu mengi ambayo yamechangia kuchukua uamuzi huo”alisema Gao.
Tayari aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Omary
Mbalamwezi ametangaza kujiuzulu na bado majibu ya kamati tendaji yakisubiriwa.
Sababu kubwa zilizochangia klabu ya Toto Afrika ya
jijini Mwanza kushuka daraja msimu wa 2012/2013 ni kukosa pesa ya nauli ya
kuwatoa uwanja wa CCM Kirumba kwenda kambini kwao nje ya uwanja wa CCM kirumba
kama kilomita mbili kutoka uwanjani.
Toto Afrika walifika kwenye hali ya kukosa mpaka
viatu vya wachezaji, mara kadhaa mwalimu wa timu hiyo John Tegete alikuwa
akilalama timu yake kutingwa na umasikini uliopitiliza hali iliyosababisha
wachezaji wa timu hiyo kujikuta wakicheza bila kupata mlo stahiki.
Tegete alipata kunukuliwa akisema kuwa, wachezaji
wake wamekuwa wakicheza huku wakiwa na njaa.
Lakini Makamu huyo amesema kuwa, Ligi Daraja la Kwanza ni ngumu kuliko Ligi Kuu, kitu ambacho kinamfanya
kujipa changamoto ya kubaki Ligi Kuu ikiwa atafanikiwa kupanda msimu ujao.
“Sisi tunakutana na wadau mbalimbali kwa lengo la
kuipandisha Toto na kwasasa hatuna shida ya pesa, ila tayari tumejipanga na tumepiga
hesabu na kubaini kuwa ili kukamilisha ligi daraja la kwanza tunahitaji
Sh150mil ambazo tunazo, pia tumepata jezi kutoka Isejele Sports ya Marekani
huku wakituahidi kutuletea basi kama tutafanya vizuri ndiyo maana tunajipanga
kufanya vizuri,”alisema Gao.
Hali hii imekuwa ikitumiwa kwa miaka kadhaa sasa
licha ya kuwa na pango ambalo limekodishwa kwa wafanyabiashara wa maduka, huku
wakiendelea kutaabika hata ofisi hawana.
Ni matarajio ya vilabu kuona mashabiki wanaviunga
mkono kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi zao ili kutunisha mfuko wa
vilabu.
Moja na dosari kubwa kwenye timu hii ni uhaba wa mashabiki wanaojitokeza uwanjani.
Kumekuwa na mwitikio mdogo wa mashabiki kwenye viwanja
kushuhudia mechi za timu yao, hali ambayo imekuwa ikiviathiri vilabu ambavyo
vingi vinavyotegemea mapato ya milangoni kujiendesha.
Wakati huohuo, kocha wa timu hiyo John Tegete alisema kuwa, pamoja na kuwapo kwa ushindani katika Ligi daraja
la kwanza, ugumu wake ni mdogo kutokana na usajili waliofanya msimu huu na
ndoto walizonazo viongozi wa sasa.
“Unajua Daraja la Kwanza ni ngumu kuliko Ligi Kuu,
ukishapanda ukafanya mikakati ya kutoshuka daraja pekee, lakini huku inatakiwa
timu moja pekee, hapo ndipo kuna kazi, ila kwasasa naona kama nafanya kazi na
watu ambao wana nia ya kuipeleka kule wanakotaka ifike” alisema Tegete.
Akizungumzia timu hiyo kukosa nafasi ya kupanda Ligi
Kuu msimu uliopita, kocha huyo alisema wameshajua upungufu wao uliosababisha
hilo, kitu ambacho wameanza kujipanga kwenye ligi yao msimu huu.
Mchezaji ambaye ameamua kurudi nyumbani, Ladislaus
Mbogo alisema kuwa, wamerudi ili kushirikiana kuipandisha timu ligi kuu kwani
ni aibu kusifika nje wakati mkoa uliozaliwa unaendelea kukosa pato linalotokana
na soka.
“Mbele ya ukuta wa Toto ukiongozwa na mimi (Ladislaus
Mbogo) hakuna atakayefurukuta wala kujaribu kupenya, naamini kikosi cha sasa
kipo imara na tumekuja kushinda tu ili kurejea ligi kuu”alisema Mbogo.
Kwa upande wa mashabiki, ni matarajio yao kuona
klabu yao ikionesha uwezo wa hali ya juu
utakawakosha mashabiki walioamua kukimbilia Ligi za Ulaya wanapohisi kuna ladha
tofauti na hapa nyumbani, huku wakitupa mikono nyuma linapokuja suala la
kuchangia pato la timu.
Bado najaribu kuangalia kama njia ipi itatatua
tatizo hili la muda mrefu ambalo limekuwa likiendelea kuwepo, Toto huanza
vizuri sana hasa wakati wakijua wanahitaji kitu ila baada ya muda wanaanza
kupitisha bakuli.
Toto Afrikans ambayo ilianzishwa mwaka 1938,
inatarajiwa kucheza mechi 48 ikiwa kundi B lenye timu za Burkina Faso, Geita Veterans SC, Green
Warriors, Kanembwa JKT, Mwadui SC, Oljoro JKT, Panone FC, Polisi Dodoma, Polisi
Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers.
Toto wamedai kuwa hawatasajili tena msimu wa dirisha
dogo kwani tayari wamewagawa wachezaji wao katika makundi matatu ambayo ni Ng’wanza,
Gemin na Sangara ambaye ni samaki anayeheshimiwa na wakazi wa kanda ya Ziwa kwa
kuwasaidia wakati wa shida yaani Mkombozi.
Huku wakidai kuwa sasa wanakuja na mfumo wa Football
yaani mchezo unaotumiwa na nchi ya Ujerumani, na kuachana na Soccer ambao ni
mfumo unaotumiwa na Uingereza.
No comments:
Post a Comment