Tuesday, September 23, 2014

Ndoto za nyasi bandia Nyamagana imetimia

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu kwa wapenzi wa soka jijini hapa kuona uwanja mkongwe wa Nyamagana ukiwekewa nyasi bandia, hatimaye ndoto hizo zimetia baada ya kuanza kwa zoezi hilo mwishoni mwa wiki.
Zoezi la uwekaji wa nyasi bandia ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu limeingia  siku ya pili baada ya kukamilika kwa mashindano ya Kombe la Meya yaliyofikia tamati siku ya Jumamosi katika uwanja huo mkongwe.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Mwesigwa Joas Selestine akizungumza wakati wa fainali za kombe la Meya aliwahakikishia wapenda soka  mkoani  Mwanza kwamba, Mwakani Michuano hiyo  lazima ifanyike katika Uwanja wa Nyamagana huku ukiwa tayari na Nyasi mbandia.
“Baada ya zoezi la uwekaji wa Nyasi bandia katika Uwanja huo kuonekana kuchukua muda mrefu licha ya mara kwa mara kuelezwa kwamba taratibu za kuuwekea nyasi bandia  zimekwisha kamilika, lakini leo nawahakikishia kwamba sasa si ndoto tena zoezi hili litaanza mara moja “alisema Selestine.
Uwanja huo mkongwe Tanzania, ulitarajiwa  uwekwe nyasi bandia kuanza mapema mwezi Mei na kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka za mkoa huu.
Kukamilika kwa uwanja wa Nyamagana, kutalifanya jiji la Mwanza kuwa mwenyeji wa michuano ya kitaifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 na wanawake chini ya miaka 20 hivyo kusaidia harakati za Tanzania kuomba uenyeji wa fainali za Afrika chini ya miaka 17.
 TFF ilipeleka mradi kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa Goal Project IV wa nyasi bandia wa dola 500,000 za Marekani katika Uwanja wa Nyamagana.
 Mradi huo ulipelekwa huko baada ya Mkoa wa Mwanza kuahidi kuchangia dola 118,000 ili kukamilisha.

No comments:

Post a Comment